VITUKO na matukio ya hatari kwenye mikutano ya CHADEMA
vimeendelea kushika kasi.
Jana Mbunge wa Ubungo, John Mnyika alinusurika kupigwa
na bomu la machozi lililorushwa na polisi waliokuwa wakizuia kufanyika
mkutano ulioitishwa na chama hicho.
Tukio hilo lilitokea katika eneo la Mabibo kwenye
viwanja vya Sahara ambapo bomu hilo lilimpata mtu aliyekuwa karibu na
Mnyika anayeitwa Thomas Jerome, aliyejeruhiwa sehemu ya paja.
Baada ya kurushwa kwa bomu hilo, polisi walitaka
kumchukua majeruhi huyo ili wamweke kwenye gari lao apelekwe hospitalini,
lakini Mnyika aliwaelekeza wafuasi wa CHADEMA kumchukua kwa madai kitendo
kilichofanywa na askari hao kililenga kuficha ushahidi wa jambo hilo.
Polisi waliokuwemo eneo la tukio waliamua kukubaliana na
matakwa ya wafuasi wa CHADEMA waliomchukua Jerome na kumpeleka hospitali
ambako hali yake inadaiwa inaendelea vizuri.
Akielezea hali ilivyokuwa akiwa katika mkutano mwingine
uliofanyika Ubungo, Mnyika alisema polisi walifika katika viwanja vya
Sahara wakiwa na magari matatu kwa lengo la kutawanya wafuasi wa CHADEMA
wasifanye mkutano wakidai haukuwa na baraka za jeshi hilo.
Mnyika alisema polisi hao walisema sababu ya kuuzuia
mkutano huo ni uwepo wa ziara ya Makamu wa Rais katika Wilaya ya Kinondoni,
hivyo walikuwa wameelekeza nguvu zao katika ziara hiyo, kwamba hawakuwa na
uwezo wa kuulinda mkutano wa CHADEMA.
“Nikiwa nimejiandaa kupanda jukwaani ndiyo polisi
walikuja kusema tuache tusifanye mkutano, nilisogea karibu na gari
kumlalamikia ofisa wa polisi kwani kitendo cha kuahirisha mkutano kwa barua
waliyoileta saa sita mchana siku ya mkutano wakati sisi tuliwapa taarifa
siku nne zilizopita ilikuwa sio haki.
“Nilimwambia ofisa huyo wa polisi kuwa nilikuwa
najadiliana kwa simu na viongozi wakuu wa Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya
Dar es Salaam na Inspekta Jenerali wa Polisi Said Mwema kumlaumu kutumika
vibaya kwa Jeshi la Polisi.
“Nilipokuwa bado najibizana naye bila fujo zozote, bomu
lilirushwa kutoka ndani ya gari ya polisi na kupita karibu na mimi
likamjeruhi mtu aliyekuwa karibu yangu, ki ukweli nimeshangazwa sana na
matumizi mabaya ya silaha za moto,” alisema.
Aliongeza kuwa katika purukushani zilizotokea baada ya
bomu kupigwa, alipoteza nyaraka mbalimbali alizokuwa amebeba kama ushahidi
kuwaonyesha wafuasi wa chama hicho hasa jinsi serikali ya CCM na wabunge
wake walivyopitisha kodi ya huduma za simu, na kodi ya laini za simu.
Slaa anena
Aidha katika mkutano huo ambao awali ulitangazwa kuwa
ungehutubiwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Willibrod Slaa, haukuweza
kuhutubiwa naye kwa kile alichosema kuwa watu wake wa usalama walimwambia
mapema hali si salama kwenye mkutano huo.
“Nilipata taarifa kutoka vyanzo vyangu kuwa polisi
walikuwa na mpango wa kuleta fujo, hivyo nikaona kwa kuwa wanatuwinda
nisingeenda kuhutubia, pengine bomu lililomkosa Mnyika lilikusudiwa kwangu
au kwa mwingine,” alisema Dk. Slaa alipozungumza na gazeti hili kwa njia ya
simu baada ya kutoonekana mkutanoni.
|