Lord
Byron mwanafalsafa na mshairi mahili wa Uingereza aliwahi kuandika maneno haya
“The great art of life is sensation, to feel that weexist even in pain.” Kwa
tafsiri isiyo rasmi ni kwamba Sanaa kubwa ya maisha ni maono, kuhisi mambo ni
madogo hata katika maumivu. Kwangu mimi nimechukulia usemi huo kama somo la
kuwafundisha watu wanaolia kwa matatizo ya aina mbalimbali.
Nafahamu
kwamba katika maisha ya kila siku hayakosekani mambo ya kuumiza. Sina shaka
kuugua, kufiwa, kukosa chakula, kusalitiwa katika mapenzi, kudhurumiwa,
kufilisika na kufutwa kazi ni mambo ambayo huzaa huzuni na machozi miongoni mwa
watu wengi. Lakini jambo la kujiuliza ni kwamba tunalia au kuhuzunika kwa
sababu matatizo yetu ni makubwa au tumekosa kufahamu kanuni ya maisha aliyoitoa
Lord!
Hebu tujiulize ni wangapi tunahuzunikia
mishahara midogo tunayolipwa makazini mwetu? Je katika huzuni hizo tulishawahi
kuwaza kwamba kuna binadamu wengine hawana kazi na wanahangaika kutafuta
shilingi mia tano kwa kuuza mihogo na karanga kwenye kona za mitaa huku wakiwa
juani?. Kama hao wapo ukubwa wa tatizo la kukosa kazi unaotuliza kila siku uko
wapi?
Uko wapi ukubwa wa tatizo la kutokuzaa wakati
kuna waliozaa na watoto wote wakafa. Kimsingi uwiano wa shida na uhimili wake
unaopatikana baina ya mtu na mtu, kamwe sifa ya huzuni hailetwi na ukubwa wa
tatizo, isipokuwa ni kukosekana kwa sanaa ya kuishi, yenye maono na hisia za
kupunguza mambo makubwa kuwa madogo.